Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Katibu Mkuu wa Hezbollah, Naim Qassem, amesisitiza kuwa harakati hiyo itaendelea kupinga uwepo wa majeshi ya Israel nchini Lebanon na haitakubali kusalimisha silaha zake kwa serikali au mamlaka yoyote ya kigeni.
Akizungumza leo, Qassem alisema kuwa usalama wa maeneo ya kaskazini mwa Israel hautakuwepo ikiwa mashambulizi dhidi ya vijiji vya Lebanon yataendelea na raia kuendelea kuuawa. Alionya kwamba kuendelea kwa mashambulizi hayo kutazidisha hali ya mvutano katika eneo hilo.
Kiongozi huyo wa Hezbollah pia alitangaza kukataa azimio la mazungumzo lililofikiwa kati ya serikali ya Lebanon na Israel, akisisitiza kuwa makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yanapaswa kuhusisha ardhi yote ya Lebanon na si maeneo maalumu pekee.
Aidha, Qassem alieleza kuwa Hezbollah haitakubali kuachana na silaha zake, akidai kuwa silaha hizo ni sehemu muhimu ya uwezo wa kujilinda dhidi ya kile alichokiita uvamizi wa Israel. Vilevile alisisitiza kuwa Israel inapaswa kuondoa majeshi yake katika maeneo yote ya Lebanon.
Katika kauli yake, Qassem alikataa ushiriki wa mataifa ya kigeni katika maamuzi yanayohusu silaha za Hezbollah na kuitaka serikali ya Lebanon kusitisha mazungumzo ya moja kwa moja na Israel. Aliongeza kuwa harakati hiyo itaendelea na mapambano yake hadi pale majeshi ya Israel yatakapoondoka kikamilifu katika ardhi ya Lebanon.
5 Juni 2026 - 18:47
News ID: 1822784
Katibu Mkuu wa Hezbollah, Naim Qassem, amesema Hezbollah haitasalimisha silaha zake wala kukubali makubaliano ya mazungumzo kati ya Lebanon na Israel, akisisitiza kuwa harakati hiyo itaendelea kupambana hadi majeshi ya Israel yaondoke kikamilifu katika ardhi ya Lebanon.
Your Comment